Kenya: Pastor Ng’ang’a Asimulia Vile Kina Dada Huwaweka Wahubiri Kwenye Mtego
Mtumishi James Ng’ang’a Maina amewataka Wakenya kukoma kumhukumu askofu wa kanisa la House of Grace David Muriithi.
Ng’ang’a alisema jamii imekuwa ikiwahukumu wanaume kila sakata la mapenzi linapotokea bila kujua walipitia majaribu. “Kwa nini mwanamke hawezi kushtakiwa kwa kumuweka mtumishi wa Bwana katika majaribu . . . Ni kwa nini?” Pasta Ng’ang’a aliuliza. Ng’ang’a alisema mwanamke aliyehusika katika sakata hiyo ndiye wa kulaumiwa akisema yalikuwa majaribu makubwa kwa Mtumishi Muriithi. “Kama ni mimi nitakushtaki kwa kuchukua mbegu yangu, mimi siwezi kubali . . . niliona huyo msichana na ni mrembo sana, alikuwa ni majaribu kweli kwa pasta,” aliongeza.
Aliwasimulia washirika kuhusu udhaifu mkubwa wa wanaume kuwa wanawake akisema hata kwenye kitabu kitakatifu kuna visa vya mabingwa walioshindwa kustahimili jazba kwa kuwaona wanawake waliowasisimua.
Alisimulia kisa cha mfalme Daudi kwenye Biblia aliyeingiwa na tamaa na kuhusika kimapenzi na mke wa mmoja wa wanajeshi wake alipoona uchi wake. “Muombee wahubiri sana, hakuna majaribu mbaya kama wanawake. Daudi mwenyewe aliona mwanamke akaingia kwenye majaribu, alikuwa ameua Goliath, ameua simba lakini alipoona mwanamke hivi akatuma na bwanake akauawe,” Ng’ang’a alisema.
Askofu Muriithi alifikishwa mahakamani na Judy Mutave aliyemshtaki akitaka kugharamia ulezi wa mtoto waliyepata naye 2019. Alisema walikuwa kwenye mahusiano kuanzia 2018 walipokutana na kupendana na kujaaliwa mtoto huyo mvulana. Sasa anataka mtumishi kulipa kodi ya nyumba, vyakula, karo pamoja na mahitaji mengine ya kumlea mtoto huyo.
Ni kisa kilichozua mjadala mtandaoni kwani Muriithi ni mtumishi wa Bwana na ana familia yake. Aidha Mutave alidai wawili hao walikutana kwenye klabu walipokuwa wakipewa moja mbili jambo ambalo limewafanya wengi kukosoa baadhi ya watumishi wa Bwana kutokana na maisha wanayoishi.
Chanzo: TUKO